UCHAGUZI Mkuu uliofanyika mwaka jana, Oktoba 30 kwa Zanzibar na Tanzania bara, Desemba 14, umeonesha ukomavu wa kisiasa, kidemokrasia na utumiaji wa haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuliko ule wa 1995 na 2000.
Tathmini ya uchaguzi huo imetolewa wiki iliyopita na Kamati ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu (TEMCO) ambayo ilifuatilia mwendo mzima kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambavyo vilikuwa vyombo vya kusimamia uchaguzi huo.
Uchaguzi wa Tanzania ambao ni hatua, ulianza tangu wakati wakuandisha wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, ambalo kwa mara ya kwanza limetumika katika uchaguzi wa mwaka jana, kwa kiasi fulani limechangia kupunguza matatizo yaliyoibuka miaka iliyopita ya kujua wapigakura.
Mwenyekiti wa TEMCO, Prof. Rwekaza Mukandala anasema kukamilika kwa uchaguzi huo ndio mwanzo na msingi wa kuanza maandalizi, marekebisho na maboresho ya uchaguzi wa 2010. Matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi hayakuwa makubwa kiasi cha kusimamisha kufanyika uchaguzi huo.
Waangalizi wa uchaguzi huo, TEMCO, wamethibitisha kuwa uchaguzi ulikuwa wa huru na haki, kwa maana kwamba licha ya upungufu uliojitokeza kwenye NEC na ZEC, bado uchaguzi huo umekuwa bora kuliko uchaguzi uliotangulia.
Uandikishaji wa wapigakura, ulifanyika kikamilifu licha ya majina mengine kujirudia, picha kujirudia, majina kuonekana kwenye vituo lakini kwenye daftari hakuna, kukosekana kwa picha na matatizo mengine, lakini kitu cha msingi ni kuendelea kuliboresha daftari.
Wadau wanaona NEC ilitumia viongozi wa kiserikali ambao kimsingi ni wa CCM, hivyo kama inataka kuboresha daftari hilo inatakiwa kuajiri wafanyakazi wake wa kudumu kwenye wilaya na mikoa au kwenye kanda ili kuendelea kuboresha daftari.
Hali hiyo ni tofauti kabisa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo hadi sasa wajumbe wa tume hiyo ni wa vyama viwili, kitu ambacho wadau wanawesema kama uhuru na demokrasia itapanuliwa maana yake itakuwa na wajumbe kutoka vyama vingine vya siasa tu na hivyo kuwa na wajumbe zaidi ya 18, kitu ambacho kitaimaliza kabisa hadhi ya kuwa tume ya uchaguzi.
Tume hiyo inatazamwa na wadau kama inatakiwa ifanyiwe marekebisho kuangalia wajumbe gani wanatakiwa kuwapo kwenye tume na wasiwe wajumbe kutoka kwenye vyama vya siasa ambao wanaingiza upenzi wa siasa na kuleta mvutano usio wa lazima ndani ya tume.
Kukua kwa demokrasia ni pamoja na utaratibu unaotumika kuteua wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, udiwani, uwakilishi, ubunge na urais. Kama hatua na mfumo wake unatawaliwa na mizengwe ni wazi wagombea watakaopatikana wanaweza wasiwe bora.
Wadau wameutazama uchaguzi uliopita kuwa wagombea wake wengi hasa wa chama tawala, wamepatikana kwa rushwa, ambayo wamedai imepakwa mafuta na sasa inaitwa takrima. Wakapingana na kifungu cha sheria hiyo na wakaomba wabunge wa chama tawala ambao ni wengi wasione aibu waibadilishe sheria hiyo na kufuta takrima.
Kuwepo kwa rushwa kulizua mtafaruku mkubwa miongoni mwa wagombea, hivyo NEC na ZEC zilikuwa na kazi kubwa kuangalia malalamiko yaliyoletwa na vyama vilivyojiona vimekosa nafasi kutokana na wapinzani kutumia rushwa kupata ushindi.
Tume hizo zilitengua baadhi ya malalamiko na kukubali baadhi yake, ambapo wapinzani wamelalamika kuwa malalamiko yao dhidi ya chama tawala mengi yanatupwa nje, huku tume zikishikiria msimamo kuwa zilitenda haki kupinga malalamiko hayo yasiyo na msingi wa ukweli.
Wadau wa masuala ya siasa nchini hasa viongozi wa vyama vya upinzani, wamezisifu NEC na ZEC namna zilivyosambaza vifaa kufika vituoni. Usambazaji na usimamizi wa vifaa vya kupigia kura umefanyika kwa makini tofauti na miaka ya nyuma ambapo vifaa hivyo vilichelewa kufika vituo vya karibu vikawahi vituo vya mbali.
Pamoja na usambazaji, tume zilikuwa wazi kwa kiasi fulani katika kuhakikisha vifaa hivyo vinafika vituoni, hata kama baadhi ya wagombea hasa wa vyama vya upinzani vililalamika kuwa kwa nini uchaguzi ulisogezwa nyuma kutoka Desemba 18 hadi 14, lakini hoja ya kwamba Serikali ilitaka watu wapate siku ya kupumzika na watumie kwa kupiga kura tu, iliwanyamazisha.
Baadhi ya wadau wamekasirishwa na uzembe ulioibuka kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura, kuchelewa kufunguliwa, kufungwa mapema na vingine kufungwa baada ya muda uliopangwa. Mtindo huo wameutazama kama ulikuwa unafanyika kama mbinu za kisiasa kukwamisha upande mmoja wa ushindani.
Wadau wamepishana mawazo kuhusu wagombea ambao walitumia pikipiki na baiskeli kutafuta kura za urais kwamba hawakuwa makini, kwani uchaguzi huo haukuja pasi na hodi ulikuwa umetangazwa siku nyingi za nyuma na wagombea wangeweza kujiandaa na hivyo kutumia vyombo ambavyo vingewafanya wasisubiri ruzuku.
Kinachoonekana hapa ambacho waangalizi wa uchaguzi, TEMCO wamekiona ni kampeni nyingi Tanzania Bara na hata Zanzibar kutawaliwa na matusi. Lugha kali na za kuhuzunisha zilivuruga nguvu za kampeni na wananchi wengi kuchukizwa na mtindo huo, ambao hauoneshi ukomavu kisiasa.
Anakiri kuwepo kwa upungufu katika baadhi ya maeneo ambayo yamechangia kutia dosari katika uchaguzi huo, lakini kwa sababu nia ni kuboresha demokrasia nchini, kinachotakiwa vyama vya siasa ni kujipanga upya kuwa tayari kukabiliana na uchaguzi ujao wa 2010.
Mada mbalimbali zilizotolewa na wasomi wa Chuo Kikuu, ambao walikuwa waangalizi wa uchaguzi nchini, zinaonesha kuridhishwa kwao na maendeleo ya demokrasia tofauti na uchaguzi wa 2005, hata kama wadau wemepinga kulinganisha huko na kudai TEMCO inatakiwa iwe na kipimo chake cha kuangalia uchaguzi.
TEMCO imetangaza na kutoa cheti cha kuutambulisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30, kwa Zanzibar na Desemba 14, kwa Tanzania Bara kuwa ulikuwa wa huru na haki, kwani matatizo yaliyojitokeza ni ya kibinadamu wala yasingeweza kubadili au kutangua hali ya uchaguzi huo.