Mahakama Kuu ya Tanzania, imeruhusu wagombea binafsi katika nafasi za Urais na Ubunge.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo jana baada ya kufuta tena ibara za Katiba namba 21 (1), 39 (1) na 69 (1) (b) zilizoingiza sheria namba 34 ya mwaka 1994 inayomtaka mtu kugombea nafasi hizo kupitia vyama vyao vya siasa.
Mahakama kuu imechukua uamuzi huo, kufuatia kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mchungaji Christopeher Mtikila aliyetaka kuwepo kwa wagombea binafsi kwa urais wabunge na madiwani.
Kadhalika, Mahakama imemwamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuzingatia ibara asili ya 21 (1) na kuongozwa na Malengo ya Msingi na Kanuni za Sera ya Serikali kuanzia jana na katika chaguzi zijazo, kuweka taratibu zitakazosimamia shughuli za wagombea binafsi.
Hatua hiyo imefikiwa siku kadhaa baada ya Mahakama hiyo ya Kikatiba kufuta vifungu vya 119 (2) na 119 (3) vilivyokuwa vinaruhusu takrima.
Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu lililokuwa likiongozwa na Jaji Kiongozi Amir Manento.
Majaji wengine ni Salim Massati na Thomas Mihayo.
Akisoma hukumu hiyo , Jaji Manento alisema Mahakama imeruhusu mgombea binafsi katika nafasi ya Urais na Ubunge sambamba na wagombea watakaoteuliwa na vyama vyao.
’Ni matumaini yetu kwamba, marekebisho yaliyoingiza sheria namba 34 ya mwaka 1994 katika ibara za 21 (1), 37 (1) (c) na 69 (1) (b) za Katiba, hazikidhi matakwa ya raia kushiriki kikamilifu katika masuala ya serikali,’ alisema Jaji Manento.
Alisema marekebisho hayo ya 11 ya sheria namba 34, hayakuwa ya lazima bali vizuizi dhidi ya haki za msingi za raia wa Tanzania kugombea katika nafasi muhimu ama kama mwanachama wa chama au mgombea binafsi.
’Tunaendelea kutangaza kuwa marekebisho hayo yalikiuka Katiba pamoja na Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu ambalo Tanzania imeridhia,’ alisema.
Alisema maazimio ya Umoja wa Mataifa lazima yazingatiwe hususan ukizingatia kwamba Tanzania haiwezi kuwa peke yake kwa kuwa ni sehemu ya Mataifa mengine.
Alinukuu tangazo la Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya raia lililoridhiwa na Tanzania mwaka 1976 ambalo ibara ya 25 inaeleza kuwa ’kila raia atakuwa na haki na nafasi bila vikwazo vyovyote visivyokuwa na sababu.’
Aidha, alisema kigezo cha sifa ya kuwa mwanachama , ndiyo ushiriki katika uchaguzi si cha lazima katika kuendeleza na kudumisha amani katika jamii pamoja na kukidhi maslahi ya watu.
Alisisitiza kuwa, marekebisho hayo ya 11 yalikuwa yanazuia raia kushiriki katika masuala ya umma kwa kuruhusu wagombea wenye vyama pekee kushiriki katika uchaguzi na hivyo kukiuka haki za msingi za raia.
Vile vile, Jaji Manento alisema ’tumeridhika kwamba mujibu maombi ameshindwa kuthibitisha hofu yake ya kuzuia wagombea binafsi katika chaguzi.’
Alisema Ibara ya tatu iliweka mfumo wa vyama vingi sambamba na mgombea binafsi.
Alisema mfumo wa wagombea binafsi ungeweza kuwepo sambamba na mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kadhalika, Jaji Manento aliamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuweka utaratbu wa usimamizi wa shughuli za wagombea binafsi.
’Tuache matakwa ya watu yafuate mkondo wake kwa kuruhusu wagombea binafsi’ alisema.
Hata hivyo, Jaji Manento alisema kuwa hawawezi kuucha uamuzi huo tu peke yake bali kwa kuzingatia maombi ya mdai na ili kuepuka kuzaliwa kwa vurugu wametoa maelekezo hayo ya kuweka utaratibu wa usimamizi wa shughuli za wagombea binafsi.
Awali, Mchungaji Mtikila kupitia Mawakili wake wawili Bw. Richard Rweyongeza na Mpoki waliiomba Mahakama Kuu kutangaza kuwa marekebisho hayo ni batili yanayokiuka sambamba na Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Raia.
Hata hivyo, Mawakili wa Serikali Bw. Ndunguru na Mwaimu walipinga hoja hizo kwa madai kuwa marekebisho hayo yalifanywa kwa manufaa ya umma na ili kuepuka vurugu na uvunjifu wa amani.
Kesi hiyo ya kikatiba ni mfululizo wa kesi aliyowahi kufungua Mchungaji Mtikila katika Mahakama Kuu mjini Dodoma kutaka mgombea binafsi.
Kesi hiyo ya awali aliifungua mwaka 1993 akitaka Mahakama Kuu kuruhusu wagombea binafsi badala ya kuwalazimisha kugombea kupitia vyama vyao.
Katika kesi hiyo, Mahakama iliruhusu mgombea binafsi.
Hata hivyo, serikali ilikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo lakini baadaye iliondoa rufaa hiyo na badala yake ilipeleka Bungeni msuada wa kurekebisha Katiba ili kupingana na hukumu ya Mahakama Kuu.
Mtikila alifanya hivyo wakati akiwa katika harakati za kusajili chama chake cha DP mwaka 1993.